Jumatano , 19th Feb , 2025

Zhang Yazhou aliyekaa kwenye siti ya abiria kwenye gari aina ya 'Tesla Model 3' mara ghafla anasikia sauti ya Baba yake aliyekuwa akiendesha gari hiyo akipayuka akisema ''Breki hazifanyi kazi''

....wakati ambao taa nyekundu zimewaka barabarani ghafla wakajikuta wameparamia gari nyingine mbili mbele na kusababisha ajali pale pale.

Baada ya tukio hili bila ya kufikiri mara mbili Zhang Yazhou alianza kuilalamikia kampuni ya Tesla mitandaoni kwa kile alichodai kwamba magari hayo hayana ubora, Zhang hakuishia hapo alienda mbali zaidi mpaka mbele ya sheria na baada ya kesi kufika mahakamani, uchunguzi ulifanyika na kubainika kwamba si kweli kwamba ajali ile ilisababishwa na breki za gari kushindwa kufanya kazi bali ni changamoto nyingine tu.

Hivyo kibao kikamgeukia Zhang na kuhitajika kuilipa kampuni ya Tesla milioni 59 kwa pesa ya Tanzania na kuomba radhi pia kwa kuichafua kampuni hiyo mtandaoni.

Si Zhang pekee ambaye amejikuta akiingia kwenye kumi na nane za Tesla, kwani miaka minne nyuma takribani watu sita ambao waliishutumu kampuni hiyo kwa hoja tofauti tofauti, walijikuta wakikumbana na mkono wa sheria na kuhitajika kuilipa kampuni hiyo baada ya kubainika kuwa madai yao hayana mashiko.