Alhamisi , 17th Nov , 2016

Mshambuliaji wa mabingwa wa Ligi Kuu Bara Yanga Saimon Msuva ambaye kwa sasa ameibua minong'ono mingi kwa mashabiki kuwa anaipenda timu ya Simba kuliko ile ya Yanga anayochezea, amenyoosha maelezo kuhusu tuhuma hizo.

Saimon Msuva akiwa KIKAANGONI

 

Akijibu maswali ya mashabiki kupitia kipengele cha KIKAANGONI cha EATV, Msuva amesema yeye siyo shabiki wa Simba kama wengi wanavyodhani, isipokuwa amelelewa kwenye familia yenye ushabiki na mapenzi kwa Simba.

"Mi sio shabiki wa Simba kwanza mjue hilo, lakini nimekulia kwenye mazingira ambayo baba yangu mwenyewe kwanza ni shabiki mkubwa wa Simba, nachezea Yanga na nina mkataba na Yanga, hivyo niko Yanga, hayo mengine hayana ukweli wowote", alisema Msuva.

Msuva aliendelea kwa kusema kuwa yeye kama mchezaji anatamani kuichezea timu hiyo kwani Simba ni timu kubwa kama ilivyo Yanga na Azam, hivyo haina ubaya wowote kwa yeye kutamani kuchezea Simba.

"Siyo kwamba sitamani kucheza Simba, Simba ni timu kama Yanga au Azam, ni timu kubwa zaidi na timu nzuri pia, naitamani Simba lakini kwa sasa watu watambue nina mkataba na Yanga na naichezea Yanga".

Aidha Msuva amewakaribisha viongozi wa Simba kufanya mazungumzo na Yanga kama watamuhitaji, na yeye yuko tayari kuhamia Simba endapo timu hizo zitakubaliana huku akiweka wazi kuwa aliyekuwa mshambuliaji wa Simba Mussa Hassan 'Mgosi' ndiye aliyemvutia yeye kuingia katika soka.