Alhamisi , 8th Oct , 2015

Imeelezwa kwamba siku ya uchaguzi mkuu utakaofanyika oktoba 25 mwaka huu, mwananchi atalazimika kupiga kura mahali alipojiandikishia, kwa mujibu wa sheria ya Taifa ya uchaguzi.

Taarifa hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi toka Tume ya Uchaguzi- Emmanuel Kawishe alipokuwa akichat moja kwa moja na mashabiki katika kipengele cha Kikaangoni Live, kinachoendeshwa na kituo cha televisheni cha East Africa Television (EATV) na East Africa Radio, kupitia mtandao wa Facebook.

Kawishe amesema mtu hataweza kupiga kura kwengine kwani sheria inatamka wazi kuwa mtu aende kwenye kituo alichojiandikishia akiwa na kitambulisho chake.

“Hamtaweza kupiga kura kwani sheria inatamka wazi kuwa uende kwenye kituo ulichojiandikisha ukiwa na kitambulisho chako, kwa mujibu wa kifungu cha 61(3)(a) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi kila mpiga kura atapigia kura mahali alipojiandikisha hivyo wanafunzi watapigia mahali walipojiandikishia, Kama haupo kwenye kituo ulipojiandikisha hutapinga kura yoyote”, alisema Kawishe.

KUHUSU VITUO VYA KUPIGA KURA
Akiongelea suala la vituo vya kupigia kura na idadi yake, Kawishe amesema kutakuwa na vituo vya kupigia kura 72000, na wameongeza idadi ili kuweza kukabiliana na tatizo la msongamano ambao unaweza ukasababisha watu kuttopiga kura.

“Wakati wa uandikishaji, ilikuwa ni kituo kimoja na kina zaidi wa watu 1000 sasa wakati wa upigaji kura kila kituo kinatakiwa kuwa na wapiga kura wasiozidi 450, hivyo vituo vya upigaji kura vinakuwa 3 hata 4 katika eneo moja walililojiandikisha,ili kuondoa msongamano vituoni siku ya kupiga kura”, alisema Kawishe alipokuwa akichati na wananchi kupitia mtandao wa Facebook.

Hata hivyo Kawishe amesema Tume itatoa kwa vyama vyote vya siasa idadi ya vituo,na katika kila halmashauri wasimamizi wa uchaguzi watatoa orodha ya vituo kwa vyama vya siasa ili wachague mawakala.

Pia Kawishe amevitaka vyama vya siasa kuchagua mawakala wanaowaamini, na pia Tume itawaruhusu kuangalia jinsi mfumo huo utakavyofanya kazi.

“Chagueni mawakala waadilifu na mnaowaamini kwani ndio watakaokuwa kituoni kuanzia mwanzo wa zoezi hadi mwisho wa kumtangaza mshindi na wataruhusiwa kuja kuona mfumo unavyofanya kazi, kuhusu ni lini Tume itawaandikia rasmi kuwajulisha muda na mahali”, alisema Kawishe.

KUHUSU TUHUMA ZA WIZI WA KURA NA KULINDA KURA.
Kuhusu suala ambalo linahofiwa na wananchi wengi wa wizi wa kura, Kawishe amesema Tume ya Uchaguzi inafuata sheria, na haikatazi kwa wananchi kulinda kura isipokuwa sheria ya uchaguzi inamtaka mtu kwenda nyumbani mara baada ya kupga kura.

“Tume haikibebi chama kimoja wala viwili, vyama vyote ni sawa mbele ya sheria, hivyo Tume inafuata sheria.sheria itafuatwa na mawakala watakuwepo kila kituo kutoka katika vyama vyenye wagombea katika chaguzi husika,Tume haikatazi mtu kulinda kura sheria inakutaka kwenda nyumbani baada ya kupiga kura”, alisema Kawishe.

Katika kukabiliana na tatizo la umeme linaloikabili nchi sasa hivi, na ambalo linaweza kuzorotesha zoezi la kuhesabu kura na kuchelewesha utumwaji wa matokeo, Tume imesema imejidhatiti kwa hilo kwa kupeleka jenereta kwa kila Halmashauri.

Pia Tume imewataka wananchi kulinda amani kwa kila mmoja kufuata sheria na taratibu, kwania amani ipo mikononi mwa Watanzania wote, na kuwahakikishia wananchi haki itatendeka kwani Tume inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba na Sheria.
Message 4 of 22