Jumatano , 22nd Mar , 2017

Msanii wa kizazi kipya Zuwena Mohamed 'Shilole' anayetamba na wimbo wa 'Hatutoi kiki' amefunguka kuwa hapendi kuzungumza lugha ya Kiingereza pasipo sababu kwakuwa ametumia gharama kuilipia lugha hiyo, na hivyo hakuna wa kumpangia kuizungumza.

Shilole ndani ya Planet Bongo

Akiwa East Africa Radio kwenye kipindi cha Planet Bongo Shilole amesema kwamba watu wanaomtaka yeye kuzungumza Kingereza wanapoteza muda wao kwa kuwa yeye alijifunza lugha hiyo kwa ajili ya maslahi yake binafsi hasa katika biashara zake.

"Dullah mimi lugha naijua sana, nimesoma kozi ya miezi mitatu, mwalimu alikuwa anakuja nyumbani kwangu kunifundisha, ukitaka kujua mimi najua kuzungumza lugha hiyo unikute kiwanja cha ndege nimechelwa ndege halafu nina show au ninapokuwa mezani nataka kuzungumza na wazungu kwa ajili ya kusaini mikataba lakini siwezi kuongea kwa kila mtu ili kudhihirisha kama naweza kwakuwa hakuna aliyenisaidia kulipa ada". Alisema Shilole.

Katika hatua nyingine Shilole amesema amechoka kutumiwa kama daraja la kuwanufaisha watu ambao wanaenda kwake kujipatia umaarufu ili wafanye mambo yao mengine ndiyo sababu ya kuachia wimbo wake mpya ambao ni salamu kwa wale wote wenye mawazo ya kutoka kupitia jina lake.

"Huu wimbo wa 'Hatutoi kiki' sijamuimba mtu mmoja ila ni salamu za watu wote ambao walikuwa wananichukulia kama daraja, kuna mtu mwingine anahangaika mwezi mmoja anataka nimfanye awe maarufu, mimi nimehangaika kulikuza jina kwa takribani miaka sita ndio maana nasema hatutoi kiki".  Alimaliza Shilole.