Hakuna wa kunipangia kunywa pombe - Dudu Baya

Wednesday , 11th Jan , 2017

Rapa mkongwe DuduBaya amefunguka na kusema kuwa hakuna mtu wa kumpangia muda wa kunywa viroba (pombe), hivyo ataendelea kunywa muda anaotaka yeye iwe asubuhi sana au mchana kwa kuwa yeye si mwajiriwa anayetakiwa kunywa pombe baada ya kazi.

Dudu Baya

Dudu Baya aliyasema hayo kupitia eNEWZ na kusema kuwa watu wanapoona yupo kimya wanadhani huenda amefulia na kusema yeye yupo busy na biashara nyingine na muda mwingi anakuwa hayuko Dar es Salaam lakini yuko poa na maisha yanakwenda safi.

"Mimi hakuna mtu wa kunipangia kunywa viroba, iwe asubuhi saa mbili, iwe saa tano asubuhi au muda wowote nitakunywa tu, Mimi siyo mwajiriwa kusema niogope kunywa nitakunywa muda nao taka mimi" Amesema 

Amesema kwa sasa maisha yake yako Mwanza na Kampala akija Dar anakuja kufanya kazi za kisanaa japo alishaamua kupotezea muziki na kufanya biashara zake mbalimbali kwa kuwa haishi kwa kutegemea mziki pekee. 

"Dudu Baya sijafulia kama watu wanavyodhani mimi na biashara zangu nyingine na muda mwingi sipo Dar es Salaam. Watanzania ndiyo tabia yao hiyo wakiona msanii haonekani wanadhani amefulia mfano watu walipoona King Crazy GK amepotea walidhani amefulia kumbe alikuwa chimbo anapiga kitabu na saizi tayari ana masters yake" alisema Dudu Baya 

Pia Dudu amesema kauli ya Darasa kuimba  kwamba 'siyo chui, simba wala mamba ngozi yake inamtosha kujigamba'  haijamsumbua kwa kuwa Darasa ni kijana wake na ni msanii ambaye amepambana kwa muda mrefu ila kwa sasa kafanikiwa hivyo anampongeza kwa mafanikio.