Jumatano , 17th Aug , 2016

East Africa Television LTD kwa udhamini wa Vodacom Tanzania, leo imezindua tuzo kubwa Afrika Mashariki, zilizopewa jina la EATV AWARDS

Meneja Mauzo na Masoko wa East Africa Television Bw. Roy Mbowe (wa kwanza kushoto) akizungumza na waandishi wa habari. Katikati ni Mkuu wa kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa Vodacom, Bi. Nandi Mwinyombella na Ndg. Aristides Kwizela (Afisa Habari, BASATA)

Akizungumza na waandishi wa habari Meneja Mauzo na Masoko wa East Africa Television LTD, Bw. Roy Mbowe, amesema tuzo hizo zitakuwa tuzo kubwa za kwanza kuanzishwa kwa Afrika Mashariki, ambazo zitaruhusu wasanii wa nchi zote za jumuia ya Afrika Mashiriki kushiriki moja kwa moja.

"Kwa kuanzia mwaka huu, tuzo za EATV zitatolewa kwa wasanii wa muziki na filamu katika nchi za Afrika Mashariki, ambapo namaanisha nchi za Kenya, Tanzania na Uganda,na lengo kuu la kuanzisha tuzo za EATV ni katika kuhakikisha kuwa tunaleta ushindani katika sekta ya sanaa, ili kusaidia kuziboresha viwango vyake na kuwa kazi nzuri zenye ubora uaoweza kushindaniwa kimataifa", alisema Bw. Mbowe.

Bw. Mbowe amesema kuwa tuzo hizo ambazo zitahusisha wasanii wa filamu na muziki, zitafanyika tar 10/12/2016, na zitaanza na vipengele kumi.

Wasanii watakaopenda kushiriki kwenye tuzo hizo wawe wamesajiliwa na BASATA, na wataji-nominate' wenyewe na kazi zao zilizotoka mwaka mmoja uliopita.

Pia Bw. Mbowe amependa kushukuru Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) kwa kuwaunga mkono na kuwapa kibali, pamoja na mtandao wa simu za mkononi Vodacom Tanzania, kwa kujitolea kudhamini tuzo hizo.

Tags: