Jumanne , 25th Sep , 2018

Mwanamuziki wa miondoko ya 'RnB' bongo, Ben Pol mwenye 'hit song' ya 'Ntala Nawe' amefunguka na kumwagia sifa muigizaji mkongwe wa filamu Monalisa, kwamba ndio msanii namba moja kutoka Tanzania ambaye anafanya kazi zake vizuri bila ya kutumia 'skendo' zozote zile.

Ben Pol

Ben Pol ameeleza hayo kupitia ukurasa wake wa kijamii wa Instagram asubuhi ya leo Septemba 25, 2018, huku akisisitiza kuwa amefarijika kufanya kazi na mwanadada huyo na kuwataka mashabiki zake wakae mkao wa kula kwa filamu ambayo wamefanya pamoja, jambo ambalo wengi wamepatwa na mashaka juu ya hilo kuwa ni kweli Ben amedhamilia kuingia bongo movie au masihara tu.

"Mona ndiye msanii wangu namba moja hapa Tanzania (ukijumlisha wasanii wote, wa muziki na 'movie' na sanaa zote kwa ujumla) anani-inspire kwa namna ambavyo anafanya kazi zake bila skendo, na kwa namna anavyojitunza, nimefarijika sana kugundua kwamba Monalisa pia ni anapenda muziki wangu 'same way' mimi ninavyopenda kazi zake, nilikuwa na ndoto ya kufanya kazi na Mona, nashukuru Mungu leo imetimia Ntala nawe movie inatoka ndani ya masaa 24", ameandika Ben Pol.

www.eatv.tv ilimtafuta Ben Pol kuzungumza naye juu ya jambo hilo, lakini kwa bahati mbaya amesema kuwa, kwa sasa ni mapema kulitolea ufafanuzi na kudai majibu ya yote yatapatikana ndani ya saa 24 katika siku ya leo.

"Ni mapema sana kusema kwamba nimeingia rasmi kwenye bongo movie au laa, ila nafikiri watu wawe watulivu katika kipindi hiki na kila kitu kitafahamika. Ila ninachoweza kusema ni kwamba nimefanya kitu na Monalisa ambacho hakuna mtu ambaye aliweza kufikiri juu ya hilo", amesema Ben Pol.

Ben Pol ni miongoni mwa wasanii wa muziki wa bongo fleva walioanza kufanya vizuri wakiwa na umri mdogo na ameweza kubaki kwenye ubora kwa miaka mingi katika ulingo huo, licha kwa sasa anaonekana kupenda kujihusisha na masuala ya uigizaji kwa namna moja ama nyingine.

Itakumbukwa miezi sita iliyopita ndani ya mwaka huu, ilisambaa 'video clip' mitandaoni ambayo inamuonyesha Ben Pol akiwa pamoja na Ebitoke wakiigiza vichekesho katika moja ya hotel zilizopo jijini Dar es Salaam.