Jumatatu , 23rd Feb , 2015

Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dkt Rehema Nchimbi amesema kuwa zoezi la uandikishaji wa Daftari la kudumu la kupiga kura kutumia mfumo wa kieletronic BVR ambalo limeanza hii leo limepokelewa kwa muitikio mkubwa wa wananchi kwenda kujiandikisha hasa vijana.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dkt Rehema Nchimbi.

Akizungumza na East Africa Radio Dkt. Nchimbi amesema kuwa muitikio huo umetokana na uhamasishaji na uelimishaji juu ya umuhimu wa kujiandikisha katika daftari hilo ili kuweza kupata nafasi ya kuwachagua viongozi wanaowataka.

Aidha Dkt. Nchimbi ameitaka Tume ya taifa ya uchaguzi NEC kujiimarisha zaidi ili zoezi hilo lisijekukumbwa na dosari kama zilizojitokeza wakati wa uandikishaji wa majaribio na kuongeza kuwa mpkaa sasa hawajapata taarifa ya usumbufu wa vifaa ila ameahidi kufuatilia suala hilo kwa ukaribu zaidi.

Dkt. Nchimbi ametoa wito kwa vijana pamoja na makundi mengine kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu kwenye zoezi hilo linalotumia mfumo wa kielektroniki wa BVR, ambao ndio utakuwa unamtambulisha rasmi mpigakura nchini.

Ameongeza kuwa uzinduzi rasmi wa zoezi hilo unatarajiwa kuzinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mizengo Pinda hapo Kesho.