Ijumaa , 8th Mar , 2019

Kiongozi wa Chama cha ACT - Wazalendo, Zitto Kabwe amesema kwamba kamwe hawataweza kuungana na Serikali katika kusherehekea sikukuu ya Wanawake kwa kuwa imeshindwa kuzuia vifo vya kina mama.

Zitto Kabwe

Zitto amelazimika kuyatoa ya moyoni baada ya jeshi la polisi kuzuia maadhimisho ya siku ya Wanawake ya Chama cha ACT - Wazalendo, yaliyotakiwa kufanyika huko Mpanda.

"Polisi wanataka tuungane na Serikali Kashaulili Mpanda!. Serikali ambayo imeshindwa kuzuiwa vifo vya mama zetu tunaungana nao vipi?, serikali ambayo kiongozi wake anatishia kupiga wanawake ‘mashangazi’ tunaungana nao kusherehekea siku ya wanawake Hatutafanya hilo" Zitto.

Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Mjini amelilalamikia Jeshi la Polisi nchini kutumika kwenye vyama vya kisiasa ambapo amesema kwamba mambo yao hayapaswi kufanyika kwenye nchi huru kama Tanzania.

"Sisi ACT Wazalendo tumezuiwa huko Mpanda, CHADEMA wamezuiwa huko Geita. Sijui lini Polisi wa Tanzania wataacha kutumika kisiasa. Haya ni Mambo ya hovyo na hayapaswi kutokea kwenye nchi huru. Kwanini Polisi iwapangie wanawake wa ACT - Wazalendo namna ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani?".

"Sisi ACT Wazalendo tulipanga kufanya mjadala kuhusu haki ya uzazi kwa wanawake kwa sababu vifo vya wanawake wajawazito vimeongezeka sana nchini tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani. Tulitaka kutoa mapendekezo ya suluhisho la hali hiyo ili kupunguza vifo vya wanawake wanapojifungua", amesema Zitto.