Mkuu wa Jeshi la zimamoto nchini Thobias Andengenye amesema kutokana na agizo la Rais lakutaka ofisi zote za serikali kuhamia mkoani Dodoma,tayari ofisi yake imewasilisha maombi kwenye mamlaka ya ustawishaji mkoani humo kwa ajili yakupatiwa eneo la ujenzi wa makao makuu ya zimamoto.
Kamanda Andengenye ameyasema hayo kwenye mahojiano maalum na kuongeza kuwa ofisi yake itahakikisha wanatekeleza agizo hilo la rais na kuanza taratibu za ujenzi wa ofisi hiyo kwa haraka kwa kuwa mkoa wa Dodoma unakuwa kwa kasi kubwa na huduma za zimamoto zinahitajika kwa kiwango kikubwa ili kuzuia majanga.
Amesema kituo kilichopo kwa sasa mkoani Dodoma hakiwezi kukidhi mahitaji ya mkoa huo hivyo wamejipanga kuongeza vituo vingi zaidi ili kuwafikia wananchi kwa haraka na kupunguza vifo pamoja na uharibifu wa mali za wananchi zitokanazo na moto,vimbunga au mafuriko ya mvua.
Kamanda Andengenye amewataka watanzania kutoa ushirikiano wa haraka pindi waonapo majanga mbalimbali yanatokea na sio kulaumu bila kuchukua hatua madhubuti zinazostahili.






