
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar Tabia Maulid Mwita
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar Tabia Maulid Mwita, ameomba radhi na kutengua kauli iliyotolewa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa, Sensa ya Filamu na Utamaduni Zanzibar, Dkt Omar Adam ya kwamba mwanaume yeyote anayetaka kusuka visiwani humo itambidi alipie kiasi cha shilingi milioni 1 ili kupata kibali cha kusuka.
Waziri Tabia amesema Katibu Mtendaji huyo aliteleza, na kwamba Zanzibar inasimamia sheria inayotaka kulinda mila na utamaduni wa Mzanzibar na ipo kanuni inayoeleza katika mipaka ya Zanzibar wanaume wa Kizanzibar kusuka ni kinyume na mila, utamaduni na desturi na yeyote atakayekiuka hayo atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kutozwa faini ama kifungo cha miezi 6.
Aidha Waziri amesema kwamba Wizara yake itaendelea kuheshimu tamaduni za watu wengine ikiwemo pia kuzingatia haki za binadamu na kwamba sheria za Zanzibar ziko palepale kwamba mila, silka na tamaduni kuendelea kulindwa.