Mkuu wa Shule Kuu ya Sheria nchini Kenya, mwanaharakati Profesa PLO Lumumba.
Profesa Lumumba ambaye pia ni mkuu wa bodi ya wakurugenzi wa shule kuu ya Sheria nchini Kenya, amesema hayo leo jijini Dar es Salaam akiwa kama mjumbe wa jopo maalumu lililoundwa na Jukwaa la Katiba kwa ajili ya kusuluhisha na kunusuru mchakato wa katiba mpya.
Katika maelezo yake Profesa Lumumba amesema idadi kubwa ya watu, wanasiasa na wadau wa katiba waliohojiwa na jopo hilo wamependekeza UKAWA warejee bungeni sambamba na kulitaka bunge hilo lijadili na kuheshimu rasimu ya katiba iliyo mbele yao pamoja na baadhi ya wajumbe wa bunge hilo kuacha lugha ya matuzi, kebehi na fedheha.
Aidha, Profesa Lumumba amezungumzia pia tatizo la rushwa kwa nchi za Afrika Mashariki na kusema kuwa tatizo ni ukosefu wa msukumo wa kisiasa katika kupambana na rushwa na ufisadi.
Kwa mujibu wa PLO Lumumba, wahusika wa rushwa wamekuwa wakiachwa pasipo kuchukuliwa hatua zozote huku wanaofikishwa mahakamani wakiwa ni maskini na watu wa kada za chini kiasi cha kufanya kesi zao zisiwe na mashiko ya kisheria.
Profesa Lumumba ametolea mfano wa nchi zilizoendelea kidemokrasia kama Ufaransa na Israel ambazo amesema zimeshuhudia waliowahi kuwa viongozi wake wakifikishwa katika mahakamani kwa tuhuma za rushwa waliyopokea au kuchukua wakati wa utawala wao.