Jumatano , 8th Jun , 2022

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ametoa siku tano kuanzia leo Juni 8, 2022 hadi Juni 12, 2022 kwa Wizara ya Kilimo iwe imeondoa pikipiki zote wizarani hapo na kuzikabidhi kwa wakurugenzi. Pikipiki hizo zimetolewa kwa ajili ya maafisa ughani kote nchini.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiwa na Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde, akiaziangalia pikipiki za maafisa ugani

Ametoa agizo hilo leo Juni 8, 2022, alipokagua Ofisi za Wizara ya Kilimo zilizopo eneo la VETA, Dodoma na kukuta pikipiki zilizotolewa kwa ajili ya maafisa ughani zikiendelea kuwepo.

“Hii haikubaliki, Wakurugenzi wote waandikiwe barua waje wazichukue, kama kuna ufungaji wa plate number utafanyika huko huko, Jumapili saa 10:00 jioni ziwe zimefika kwa wahusuka,"ameagiza Waziri Mkuu

Amesema tayari Rais Samia alishazikabidhi kwa ajili ya kupelekwa kwa maafisa ugani, hivyo kitendo cha pikipiki hizo kuendelea kubaki katika eneo hilo hakikubaliki.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Profesa Siza Tumbo, amemhakikishia Waziri Mkuu kwamba wamepokea maelezo hayo na watayafanyia kazi.