Ijumaa , 16th Jan , 2015

Kamati ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Mazingira imeitaja Wizara ya Ardhi kuwa kinara wa urasimu na ukiukwaji wa taratibu na sheria za ardhi kiasi cha kuchochea migogoro na ucheleweshwaji wa mikataba ya ardhi

mwenyekiti wake Mhe. James Lembeli

Kamati ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Mazingira imeitaja Wizara ya Ardhi kuwa kinara wa urasimu na ukiukwaji wa taratibu na sheria za ardhi kiasi cha kuchochea migogoro na ucheleweshwaji wa mikataba ya ardhi inayotekelezwa na mashirika na idara za serikali.

Akiongea mara baada kamati hiyo kutembelea eneo la uwekezaji wa shirika la nyumba NHC Mbezi luguluni jijini Dar es Salaam mwenyekiti wake Mhe. James Lembeli ametaja mapungufu hayo kuwa ni pamoja na kugawa ardhi mara mbili, kugawa maeneo ya wazi, hifadhi za mito, barabara, mabwawa pamoja na kukiuka sheria ya uendelezaji wa ardhi kwa kipindi cha miaka mitatu na kusababisha watu kuhodhi maeneo makubwa kwa muda mrefu bila ya kuyaendeleza kinyume cha sheria.

Kwa upande wake katibu mkuu wizara ya ardhi nyumba na makazi Bw. Alphayo Kidata pamoja na kukiri mapungufu hayo ameeleza kuchochewa na baadhi ya watendaji katika halmashauri, manispaa na wizarani kushindwa kusimamia sheria na kanuni na kujikuta wakiiweka wizara katika wakati mgumu wa kutatua migogoro akiahidi kusimamia vyema sheria kwa ufumbuzi zaidi.

Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa eneo la uwekezaji mkurugenzi wa biashara wa shirika la nyumba NHC David Shambwe pamoja na kueleza kutekeleza miradi ya zaidi ya bilioni 400 kwa wakati mmoja nchini kote ameelezea uwekezaji wa Luguruni kuwa wa kituo kikubwa cha biashara, makazi na usafirishaji kama hatua yake ya kupanua huduma za jiji kutoka katikati ya jiji la Dar es salaam na hivyo kupunguza msongamano wa kihuduma.