Jumatano , 30th Nov , 2016

Kuelekea siku ya UKIMWI duniani Desemba 01, Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza mwongozo mpya wa kujipima Virusi Vya Ukimwi, VVU kwa lengo la kupanua upatikanaji wa huduma hiyo na uchunguzi wa virusi hivyo.

Kifaa kinachotambulika kwa jina la OralQuick kilichoundwa nchini Marekani sasa chaweza kutumika katika kupima virusi vya UKIMWI kwa kuweka katika ufizi.

 

Mwongozo huo unahusisha mtu kuchukua vitendanishi na kujipima kwa kutumia majimaji ya mwilini au damu kutoka kidoleni na kubaini iwapo ana virusi au la, na majibu anapata ndani ya dakika 20 au chini ya hapo.

WHO inasema iwapo majibu yanakuwa chanya, mtu huyo analazimika kwenda kituo cha afya na kusaka uhakika wa matokeo hayo ambapo ikiwa yatathibishwa, atapatiwa ushauri nasaha na huduma nyingine za matibabu ikiwemo dawa.

WHO inasema mwongozo mpya ni muhimu kwa kutafungua milango zaidi kufikia watu wengi na ni njia mojawapo ya kuwapatia watu uwezo juu ya afya zao na kusogeza huduma karibu na wananchi.