Jumanne , 5th Sep , 2023

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega, amesema Wizara yake itatumia Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula (AGRF), kuitangazia dunia dhamira ya dhati ya serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuzalisha na kuuza kwa wingi protini itokanayo na mazao ya mifugo na uvuvi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega

Waziri Ulega amebainisha hayo Septemba 05, 2023 jijini Dar es Salaam kunakofanyika mkutano huo ambapo amesema kuwa kwa kuanzia Wizara yake imeona fursa ya soko la mayai kwenye nchi zenye mahitaji makubwa ya chakula. 

"Tunafahamu kwa sasa mashirika ya kimataifa yamekuwa yakipelekea mazao ya nafaka kwenye nchi hizo kwa hiyo na sisi tumeiona fursa ya kupeleka mazao yatakayoongeza protini ambapo tunataka sasa wafugaji wetu waongeze kiwango cha uzalishaji wa mayai na ikiwezekana tuyachemshe kabisa ili kuyaongezea thamani na kuyapeleka huko," Amesema Mhe. Ulega.

Waziri Ulega ameongeza kuwa kwa sasa nguvu kubwa ya uzalishaji imeelekezwa kwa wanawake na vijana ambapo amebainisha kuwa anaamini kama kundi hilo likiwezeshwa mtaji ya kutosha na teknolojia ya kisasa litaongeza kasi ya uzalishaji wa mazao yote yatokanayo na sekta ya Mifugo na Uvuvi na hivyo kukidhi soko la ndani na nje ya nchi.

Mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Mifumo ya Chakula (AGRF) unafanyika kuanzia leo septemba 05-08, 2023 ambapo mada mbalimbali zinazolenga kuboresha uzalishaji na masoko ya mazao yatokanayo na sekta ya kilimo kwa ujumla zitawasilishwa, kujadiliwa na kufikiwa maamuzi.