Alhamisi , 7th Mar , 2019

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Mawaziri wa Kilimo, Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mifugo na Uvuvi na Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wakutane na wafanye mapitio ya taasisi zao na kuangalia maeneo yanayogongana kiutendaji ili kila mmoja abaki na jukumu lake.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya kuwepo kwa malalamiko na manung’uniko kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara ambao wamedai kuwepo kwa muingiliano wa majukumu ya kiutendaji ya taasisi za (TFDA) na (TBS), hivyo kuwasababisha washindwe kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Waziri Mkuu amesema taasisi hizo zinashughuli ambazo zinaingiliana na kusababisha malalamiko kwa wateja wao, ambapo ametolea mfano suala la kudhibiti ubora wa bidhaa ambalo linafanywa na TFDA na TBS kwa mujibu wa sheria.

Kutaneni pitieni maelekezo ya Serikali yanayoelekeza namna ya kuzifanya taasisi hizi na zingine zinazofanya shughuli zinazofanana zilizo katika wizara zenu bila kusanau Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (blue print). Ifikapo tarehe 30 mwezi huu niwe nimepata mapendekezo yenu,” amesisitiza.

Pia, Waziri Mkuu amewataka waangalie namna ya kuwahisha majibu ya vipimo vya bidhaa wanazoletewa na wateja, kama watakuwa wamekamilisha kabla ya siku za kisheria wawajulishe wateja wao na kuhusu sampuli ambazo zitakuwa hazijaharibika wakati wa vipimo wawarudishie.