Jumatatu , 19th Feb , 2018

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua mradi wa maji katika kijiji cha Bwasa katika mji wa Nansio wilayani Ukerewe na kuuagiza uongozi wa wilaya hiyo kuhakikisha maji hayo yanatoka wakati wote na mradi huo unakuwa endelevu.

Waziri Mkuu alizindua mradi huo wakati akiwa katika siku ya nne ya ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza na kusema serikali imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama nchini.

Baada ya kuzindua mradi huo, Waziri Mkuu alizungumza na wananchi wa mji wa Nansio kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Getrude Mongella, ambapo amesema mradi aliouzindua katika kijiji cha Bwasa ni sehemu ya mradi wa maji wa Kazilankanda utakaohudumia vijiji 13 vya wilaya hiyo.

"Mradi huu unagharimu shilingi bilioni saba na unatekelezwa katika vijiji vya Muhula, Mahande, Namasabo, Namagondo, Kazilankanda, Malegea, Igalla, Kigara, Lutare, Busunda, Bwasa, Buhima, Hamuyebe  na utahudumia wakazi  68,038 pindi utakapokamilika", amesema Kassim Majaliwa.

Pamoja na hayo, Waziri Mkuu ameendelea kwa kusema "mkataba wa mradi ulisainiwa Machi 2013 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Aprili, 2018, ambapo hadi sasa jumla ya shilingi bilioni 5.637 sawa na asilimia 78.26 tayari zimeshatumika na mradi umekamilika kwa asilimia 92 na tayari baadhi vijiji vimeanza kupata maji".

Aidha, Waziri Mkuu amesema serikali inatekeleza kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, inayolenga kuwaondolea wananchi tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.

Kwa upande mwingine, Waziri Majaliwa amewaambia wananchi kuwa serikali ya awamu ya tano ina mikakati mizuri inayolenga kuondoa tatizo la maji kote nchini ili kusaidia wananchi hao hasa wanawake kutumia muda mwingi kufanya kazi za maendeleo kuliko kutafuta maji.