Jumatano , 17th Aug , 2022

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ametatua mgogoro wa ardhi uliodumu kwa miaka mitatu katika eneo la Boko-Dovya, wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam baina ya Aloyce Mwasuka na Salutari Massawe.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Katika mgogoro huo unaohusisha viwanja namba 393, 395 na 370 kwenye kitalu G (Boko Dovya) vilivyoko njiapanda ya Mbweni, Massawe alijenga ukuta ambao ulikuwa unazuia matumizi ya barabara na hivyo kumfanya Mwasuka apitie kwa jirani yake Bi. Oliver Semuguruka (kiwanja na. 395) ili aweze kufika nyumbani kwake (kiwanja na. 393).

Akizungumza na watendaji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wa wilaya ya Kinondoni katika kikao alichokiitisha leo Agosti 17, 2022, ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na hatua aliyoichukua mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe ya kusimamia uvunjaji wa ukuta huo ili kupisha eneo la barabara.

"Ninakushukuru mkuu wa wilaya na timu yako kwa kuchukua hatua tangu jana ili kusimamia haki ya wananchi wasio na uwezo, haki ni ya kila mmoja, mwenye uwezo na asiye na uwezo, ile barabara iboreshwe ili wananchi wote wanufaike," amesema Waziri Mkuu

Waziri Mkuu amesema hatua hiyo inaenda sambamba na utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan, aliyowapa wasaidizi wake akitaka wahakikishe kuwa wananchi hawapati shida kwenye maeneo yao.