Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
Waziri Mkuu ametoa pongezi hizo wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya wiki ya huduma ya fedha yanayofanyika kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha baada ya kutembelea banda la maonesho la benki ya Exim Tanzania.
"Niwapongeze sana kwa jitihada mnazoendelea kuzifanya katika kupanua zaidi huduma zenu, hata hivyo jitihada zaidi zinahitajika ili hizi huduma nzuri mnazoendelea kuzitoa ziwafikie wananchi wengi zaidi hususani waliopo pembezoni huko ambao bado hawajafikiwa na huduma rasmi za kifedha," amesema Waziri Mkuu
Waziri Mkuu Majaliwa ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa watoa huduma za kifedha nchini kuhakikisha wanaendelea kutoa elimu ya fedha kwa umma sambamba na kupunguza gharama za uendeshaji wa huduma hizo zikiwemo riba na ada ili wananchi wengi watumie huduma za fedha zilizo rasmi.
Akiwa kwenye banda hilo Waziri Mkuu alipata wasaa wa kupata maelezo kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo kutoka kwa Meneja Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo, Bi Kauthar D’Souza ambae pamoja na kuelezea baadhi ya huduma za kifedha zinazotolewa na benki ya Exim Tanzania pia alielezea kuhusu mkakati wa benki hiyo katika kujitanua katika maeneo mbalimbali nchini.
Awali akielezea kuhusu huduma za benki ya Exim Tanzania mbele ya Waziri Mkuu Majaliwa, Bi Kauthar alisema licha ya jitihada za benki hiyo katika kujitanua zaidi nchini ambapo hadi sasa ina mtandao wa matawi 33 na mawakala 1500 nchi nzima, bado mkakati wake ni kuwekeza zaidi katika utoaji wa huduma kupitia ubunifu wa kidijitali ili kutoa masuluhisho ya kibenki yanayofaa na salama kwa wateja wake.