Jumapili , 30th Jun , 2024

Waziri wa Nchi,  Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene, amesema aliyekuwa Diwani wa Viti Maalum wa Jimbo la Kibakwe, Maria Kigosi amekufa kifo cha kawaida na hakuna mtu yeyote aliyempa sumu.

Pia, amesema marehemu hajafa kifo cha ghafla kama inavyodaiwa bali alikuwa anaumwa na amefia hospitali ya Tumaini wilayani Mpwapwa.

Ametoa kauli hiyo leo wakati akishiriki ibada ya mazishi iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Kibakwe, Tarafa ya Kibakwe, Halmashauri ya wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma.

Amefafanua kuwa marehemu alikuwa anaumwa kwa muda mrefu ambapo watu wa karibu akiwemo mume wa marehemu anatambua kuwa mke wake alikuwa akiumwa kwa muda mrefu na amekiri kuwa  alikuwa mbioni kumpeleka Mke wake katika hospitali kubwa.

 "Lakini huku mtaani kumekuwa na maneno mengi kuwa marehemu alipewa sumu na wameenda mbali zaidi kwa kuwataja  wahusika waliompa sumu na  sumu hiyo ilitoka kwa nani,  nataka niwahakikishie sio kweli huo ni uongo mtupu," ameng’aka Mhe. Simbachawene

Aidha, ameweka bayana kuwa serikali imefanya utafiti wake kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na familia yake hususani mume wake na  kujiridhisha kuwa marehemu Maria hakulishwa sumu.

Hata hivyo Mhe.Simbachawene amesema madaktari wameweza kujua alichokuwa akiumwa ndani ya muda mfupi aliokimbizwa hospitalini.

Kufuatia hatua hiyo, Mhe.Simbachawene amewataka Madiwani,  Wananchi wa Kibakwe pamoja na familia yake kwa ujumla  kupuuza uvumi huo la sivyo wataanza kugombana pamoja na kudhalilishana kwenye jambo lisilo na chembe chembe yoyote ya ukweli.

Aliyekuwa Diwani wa Viti Maalum Maria Kigosi alifikwa na umauti siku ya Jumatano saa 10:00 usiku mara baada ya kuanza kujisikia vibaya na kukimbizwa hospitali ya Tumaini Wilayani Mpwapwa.