Alhamisi , 12th Jun , 2014

Serikali ya Tanzania imesema itahakikisha katika sera ya mafuta na gesi inayokuja, wazawa katika maeneo yanakochimbwa mafuta na gesi wanapewa kipaumbele cha kwanza katika kuwawezesha kiuchumi.

Moja ya mitambo inayotumika katika utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi katika kina cha bahari kuu.

Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Ngosi Mwihava wakati wa mkutano wa pamoja uliowakutanisha watafutaji wa mafuta kutoka ndani na nje ya nchi.

Mhandisi Ngosi amesema tayari kwa sasa wameshaanza kutekeleza suala hilo na makampuni kadhaa ya madini na kwamba katika uandaaji wa sera hiyo watashirikisha wananchi kwa kuhakikisha kwamba sekta za Miundo mbinu, Maji, Afya na Elimu watanufaika nazo.

Wakati huohuo, Wizara za fedha katika nchi za Afrika za Mashariki zinatarajia kuwasilisha hotuba za bajeti za wizara hizo ambapo Nchini Uganda Bajeti ya Takribani Tril 14 itawasilishwa na waziri wa fedha Maria Kiwanuka, huku nchini Kenya ikiwasilishwa na Henry Rotich na nchini Tanzania bajeti inategemea kusomwa na Bi. Saada Mkuya.

Wananchi katika nchi hizo wanatarajia bajeti hizo zitaleta ahueni kwa maisha yao ya kila siku.