Jumatano , 22nd Jun , 2022

Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Ngollo Malenya amesema baadhi ya Wananchi Kijiji cha Mzelezi Wilayani Ulanga wamempiga na kumjeruhi  Kaimu Afisa Tarafa ya Ruaha, George Kayola (36) wakati Afisa huyo akiwa katika majumu yake.

George Kayola alikuwa akitekeleza maagizo ya DC aliyoyatoa katika ziara yake ya kikazi Kijijini hapo ya kuzuia Watu wanaofanya shughuli za uchimbaji wa madini pembezoni mwa Hifadhi ya Barabara iliyo chini ya TANROADs.

DC Ngollo amesema Afisa huyo akiwa katika kuwazuia Watu waliokuwa wamekaidi agizo hilo ndipo mapambano dhidi yake yalianza na kupelekea Kujeruhiwa mkononi kwa kuchanwa na silaha yenye ncha kali na pia akajeruhiwa maeneo ya bega lake la Kulia. 

“Tukio limetokea June 17,2022, na tayari Jeshi la Polisi Wilaya ya Ulanga  linawashikilia Watu wawili ambao ni Edwin Luciana Dendelege (38) na Charles Orestus Madonga wakitajwa kuhusika na tukio hilo, kwa sasa Mgonjwa amelazwa Hospitali ya Rufaa ya Mt.Fransisko, Ifakara”

DC Ngollo amelaani vikali kitendo hicho cha Wanachi kujichukulia hatua mkononi na badala yake amesisitiza wafuate sheria na taratibu dhidi ya Watumishi wa Serikali wanapohisi wanawakosea.