Jumatano , 6th Jul , 2016

Taasisi za kifedha nchini zimetakiwa kubuni mbinu mbadala zitakazo wasaidia watanzania kuwa na kipato cha ziada ili waweze kujiunga na kumudumu kulipia gharama za bima mbalimbali.

Wito huo umetolewa na Msajili wa Hazina Bw. Laurence Mafuru alipotembelea maonyesho ya biashara ya kimataifa Sabasaba na kusema kuwa taasisi hizo zisisubiri watanzania kujiunga nao na badala yake wawape mbinu za kujitegemea kiuchumi.

"Kwa maisha ya wananchi wa chini kujiunga na bima ni ngumu, kwani mtu anafikiria nilipie ada, kodi ya nyumba na matumzii mengine na malipo ya bima anayaweka pembeni kwani pesa inakuwa imeisha, lakini wangekuwa na kipato cha ziada basi angeweza kumudu," amesema Mafuru.

Mafuru amesema kuwa, ni ngumu kwa wananchi wa kipato cha chini kuweza kulipia gharama za ada, nyumba na shuguli mbalimbali muhimu na baadaye kuwa na akiba ya ziada kwa ajili ya malipo ya bima.

Aidha, Laurence pia amewataka wataalamu wa fedha kutoa elimu ya kutosha kwa jamii juu ya umuhimu wa bima za afya na zinginezo katika ustawi wa maendeleo yao kiujumla.