
Tatizo la kukatika katika kwa umeme mara kwa mara linaoendelea katika maeneo mengi ya jiji la Arusha limeanza kuathiri huduma za kijamii zikiwemo huduma za afya hususani kwenye vituo vya afya vinavyotoa huduma ya upasuaji na huduma za kujifungua kwa kinamama wajawazito.
Kituo cha afya cha Themi ni moja ya vituo vilivyoanza kuonja adha hiyo ambapo mganga mfawidhi Dkt Miraji Kyande anasema wamekuwa wakilazimika kutumia taa za chemli kuwasaidia kinamama wakati wa kujifungua.
Ni baada ya kuona changamoto hiyo kampuni inayosambaza umeme wa jua ya mobisol imetoa msaada wa mtambo wa umeme wa jua kwa kituo hicho cha afya kama njia mojawapo ya kuokoa maisha ya kina mama na watoto, msaada ambao kaimu mganga mkuu wa jiji la Arusha Japhet Kivuyo anasema umefika wakati muafaka.
Akipokea msaada huo Diwani wa kata hiyo ya Themi Denis Kinabo anasema pia utapunguza usumbufu kwa wagonjwa wanaohitaji huduma za maabara ambao majibu yao yalikuwa yanasubirishwa mpaka vipimo vipelekwe kwenye hospitali ya mkoa.