Jumamosi , 28th Nov , 2015

Waziri Mkuu wa Tanzania Majaliwa Kassim Majaliwa hii leo amewasimamisha kazi watumishi wengine watatu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao jana iliamriwa kwamba watahamishiwa mikoani.

Waziri Mkuu, Mhe.Kassim Majaliwa akiwasalimia Kamishna aliyesimamishwa kazi,Rished Bade wakati alipotembelea Bandari ya Dar es salaam kitengo cha Ukusanyaji mapato

Waziri Mkuu wa Tanzania Majaliwa Kassim Majaliwa hii leo amewasimamisha kazi watumishi wengine watatu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao jana iliamriwa kwamba watahamishiwa mikoani.

Mhe. Majaliwa amesema ili kupisha uchunguzi zaidi wa tuhuma zinazowakabili watumishi Anangisye Mtafya, Nsajigwa Mwandengele na Bw. Robert Nyoni kama ilivyo kwa wenzao sita waliosimamishwa kazi jana (akiwemo aliyekuwa Kamishna Mkuu), nao pia hawaruhusiwi kusafiri kwenda nje ya nchi hadi uchunguzi utakapokamilika.

Waziri mkuu amemuagiza Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Dkt. Philip Mpango atekeleze maagizo hayo kwa kuwaandikia barua watumishi hao.

Jana mchana, waziri mkuu alifanya ziara ya kushtukiza kwenye bandari ya Dar es Salaam akiwa na nia ya kukagua namna shughuli zinavyoendelea kwenye bandari hiyo hasa kwenye maeneo ya kupokelea mizigo kutoka nje ya nchi na kubaini upotevu wa makontena 349 yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 80/-.