Ijumaa , 1st Aug , 2014

Watuhumiwa 19 wa milipuko ya mabomu na umwagiaji tindikali wamefikishwa mahakamani Arusha na kusomewa mashitaka yakiwemo ya mauaji.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha

Watuhumiwa  19  wanaohusishwa   katika  mtandao  wa  kulipua  mabomu katika  mikusanyiko   na  kuwamwagia tindikali viongozi  wa  dini  wamepandishwa kizimbani leo katika mahakama  ya hakimu  mkazi  mkoa  wa   Arusha  na kusomewa  mashitaka  mbalimbali  yakiwemo  ya mauaji.

Watuhumiwa   hao   ambao  wameunganishwa  na  wenzao   zaidi  ya   20 waliokwishafikishwa  kwenye  mahakama hiyo   kwa  tuhuma  hizo  wamefikishwa  mahakamani  hapo  chini  ya ulinzi   mkali   wa   polisi   ambao   hajawahi   kuonekana   katika siku  za  hivi  karibuni. 

Tofauti    na ilivyokuwa  hapo  awali    ulinzi katika mahakama hiyo  uliiimarishwa  kwa kiasi  kikubwa   kuanzia   mapema  alfajiri  ambapo  watu wote  waliokuwa  wanaingia   kwenye  lango la  mahakama  hiyo  walikaguliwa  na  vifaa  maalumu,  utaratibu  ambao  ulifuatwa  na watu  wote  bila  kujali  nyadhifa  zao   wakiwemo  watendaji  wa  mahakama hiyo. 

Baada  ya  kufikishwa  mahakamani hapo   mbele  ya hakim  Devota  Msofe  aliyekuwa anasaidiwa  na  waendesha  mashtaka  Agustino  Kombe, Felexs  Kwetukia  na  Maselina Mwamunyange,   washtakiwa  hao walisomewa   mashtaka   yanayowakabili    kwa  makundi,  jinsi  wanavyodaiwa   kuhusika   na   madhara   yaliyosababishwa   na   makosa  hayo.  

Miongoni  mwa  mashitaka  waliyosomewa  ambayo   kila  mmoja  alihusishwa kwa  namna moja  ama  nyingine  huku   baadhi yao   wakijikuta  wakitajwa  karibu  kwenye  makosa yote  ni pamoja  na shtaka  la  mauaji , kujihusisha  na  vitendo vya  kigaidi , kukusanya silaha   yakiwemo  mabomu , kuyasafirisha  na kisha  kuyatumia  kuua  na  pia  kufadhili vitendo hivyo    kwa  kutoa  fedha   na ushirikiano  wa  kuvitelekeza.

Mashtaka   mengine  ni  pamoja  na  kushawishi   na  kuhamasisha  vijana  kujiunga  na vikundi  vya ugaidi, kuhifadhi   zana  na silaha  kwa lengo  la  kufanya ugaidi   na kuzitumia  kutekeleza  vitendo hivyo.

Kesi ya watuhumiwa  hao  ambao  wote  wanahusishwa  na  matukio yote  ya   milipuko  ya mabomu  na kuwamwagia  viongozi  wa  dini   tindikali   vilivyowahi kutokea   mkoani Arusha  itatajwa tena  tarehe 15/08/2014   na washtakiwa wote  wamerudishwa  rumande ambapo kwa  mujibu  wa sheria kesi  yao  haina  dhamana