Ijumaa , 5th Jun , 2015

Wanafunzi sita wa sekondari ya Makatekista na mkuu wa shule hiyo wamefariki dunia na wengine 26 kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutumbukia kwenye korongo na kuwaka moto.

Wanafunzi  sita wa sekondari ya makatekista  na  mkuu wa sekondari hiyo Padri Hyasinti Kawonga wamefariki dunia na wengine26  kujeruhiwa kati ya hao wanne hali zao zikiwa mbaya  baada ya  ya gari aina ya Land Rover One-Ten kutumbukia kwenye korongo na kuwaka   moto katika kata ya Kigonsera wilayani Mbinga  mkoani Ruvuma.

EATV imefika  eneo la tukio Kigonsera wilayani Mbinga mkoa wa  Ruvuma  na kushuhudia  kijiji  cha Kigonsera kikiwa  katika hali ya simanzi ambapo mganga mfawidhi wa kituo cha afya Kigonsera Dkt Patrick Mhagama amesema wamepokea miili saba na majeruhi  ishirini na  sita.

Dkt. Patrick pia amesema kwamba miili imeungua vibaya kiasi  cha kushindwa  kutambulika baada ya gari hilo kuwaka moto .

Mashuhuda wa tukio  hilo   wanasema ajali hiyo ilitokea baada ya kufeli breki na dereva ambaye alikuwa marehemu Padri Hyasinti Kawonga  akakata kona ndipo alipoingia kwenye korongo na ikatokea shoti na gali likawaka moto.

Hilo ni tukio la tatu katika miaka tofauti kuua watu saba ambapo kuna wanajeshi saba walikufa kwa ajali  ya  gari na kufuatiwa  na ajali  ya maji ilioyoua watoto saba waliosombwa na maji katika kata ya Kigonsera..

Mwenyekiti wa kitongoji cha Misheni  katika kata ya Kigonsera bw. John  Kafarapia  amesema ni pigo kufiwa  na padri Kawonga aliyekuwa mkuu wa shule ya sekondari ya makatekista na mfadhiri wa wananchi mbalimbali.