Baadhi ya wakazi wa mabatini Mwanza wakifuatilia kazi ya uokoaji
Watu wanne wa familia mbiili tofauti wakazi wa mtaa wa Nyerere A, eneo la Mabatini jijini Mwanza wamefariki dunia usiku wa kuamkia leo baada ya kuangukiwa na mawe wakiwa wamelala.
Tukio hilo limetokea majira ya saa Nane usiku wakati mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali pamoja na radi ilipokuwa ikinyesha.
EATV imefika katika eneo la tukio na kushuhudia wananchi wakishirikiana na jeshi la uokoaji na zimamoto pamoja na askari polisi wakiendelea na kazi ya kufukua miili iliyonasa chini ya jiwe kubwa.
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Nyerere A, mabatini jijini Mwanza Hassan Maulid amewataja waliofariki dunia kuwa ni Sayi Otieno na Kwinta Kweko ambao ni mume na mke huku watoto wawili Kelfine Masalu na Emanuel Joseph wa familia ya Bw.Joseph William nao pia wakipoteza maisha baada ya chumba walichokuwa wamelala kuangukiwa na jiwe lililoporomoka kutoka juu mlimani.
Kaimu kamanda wa jeshi la uokoaji na zimamoto mkoa wa Mwanza inspekta Augustino Magere amewashauri wakazi wa jiji la Mwanza waishio maeneo ya milimani kuchukua tahadhari ili kuepusha maafa kama yaliyojitokeza.
Wakisimulia tukio hilo katika hali ya majonzi na simanzi, baadhi ya wakazi wa mtaa huo wa Nyerere A, wanaeleza namna walivyoupokea msiba huo mkubwa.
Huyu ndiye mtoto pekee aliyenusurika kifo baada ya wazazi wake kufariki dunia kufuatia nyumba yao kuangukiwa na jiwe kubwa.