Ijumaa , 1st Mei , 2015

Zaidi ya watoto 7000 kutoka kaya masikini wilayani Chamwino mkoani Dodoma wamenufaika na mpango wa kunusuru kaya masikini unaoendeshwa na mfuko wa taifa wa maendeleo ya jamii TASAF.

Mratibu wa TASAF wilayani Chamwino Christina Mtwale.

Mradi huo umeweza kulipia ada mashuleni pamoja na kupatiwa huduma za matibabu bure kwa watoto wenye umri chini ya miaka 5

Mratibu wa TASAF wilayani Chamwino Christina Mtwale amesema watoto hao wanafadhiliwa kupitia ruzuku inayotolewa na mfuko huo kupitia mpango wa kuzinusuru kaya masikini na unatekelezwa katika vijiji 50 ambapo wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari hulipiwa ada ya masomo huku watoto walio chini ya umri wa miaka 5 wakipatiwa huduma ya kliniki na matibabu bure .

Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Chamwino Mohamedi Omary, amewataka watendaji wa vijiji na kata kuusimamia mpango huo kwa makini ili uwe na tija huku akionya kuwa halmashauri hiyo haitasita kumshughulikia mtu yeyote atakayebainika kutumia fedha hizo kinyume na makusudio.

Nao baadhi ya madiwani na watendaji wamezungumzia mpango huo na kusema ni mkombozi kwa wakazi wa wilaya hiyo ambayo imekuwa ikikumbwa na ukame wa mara kwa mara ambao kwa kiasi kikubwa umechagia kushusha vipato katika kaya nyingi na kusababisha watoto wengi kushindwa kupata huduma za msingi ikiwemo elimu, afya, chakula na malazi bora.