Alhamisi , 11th Feb , 2016

Mamlaka ya bandari (TPA), imezisimamisha kazi kampuni 210 za uwakala wa kutoa mizigo bandarini kutokana na kushindwa kuwasilisha vielelezo vya malipo waliyoyafanya wakati wa kutoa mizigo.

Kaimu Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Bi. Janeth Ruzangi

Kampuni hizo zinatuhumiwa kuhusika kutorosha makontena 11,884 na Magari 2019 kutoka bandari kavu (ICD) saba za Azam za jijini Dar es salaam bila kulipiwa ushuru wa bandari, hivyo kuipotezea serikali mapato ya shilingi bilioni 48.

Meneja wa mawasiliano wa TPA, Janeth Ruzangi amesema hayo jana na kusema kuwa mawakala hao wamesimamishwa baada ya kupewa muda wa kuwasilisha nyaraka hizo mwishoni mwa Desemba mwaka jana Kushindwa.

Ruzangi amesema mawakala hao 210 ni kati ya mawakala 280 ambao waziri Mbarawa aliwataka kuwasilisha nyaraka za malipo sahihi kwa mizigo ambayo waliiondoa ndani ya bandari hiyo kuanzia Julai hadi Desemba mwaka jana.

Katika maelezo yake meneja huyo mawasiliano amesema mara baada ya kampuni hizo za uwakala wa forodha zitakapowasilishwa vielelezo hivyo vya malipo bandari itawafungulia na kuendelea kufanya nao biashara.