Alhamisi , 20th Mar , 2014

Jeshi la polisi kanda maalum ya Dar es Salaam nchini Tanzania limefanikiwa kuwakamata watu wanne ambao walikuwa wakijiandaa kusafirisha dawa za kulevya zilizokuwa zimefichwa katikati ya vitabu kama kifurushi cha kusafirisha nje ya nchi.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumya Dar es Salaam Kamishna Suleiman Kova amesema watu hao wamekamatwa katika ofisi za Kampuni ya kusafirisha vifurushi za DHL zilizopo Mtaa wa Sam Nujoma Jijini Dar es Salaam.

Watu hao ambao watatu kati yao ni raia wa Nigeria na mmoja mwanamke raia wa Tanzania wamekamatwa na dawa hizo za kulevya wakijiandaa kwenda nchini Liberia na Afrika Kusini.

Madawa hayo ya kulevya aina ya Heroin na Cocaine yanakadiriwa kuwa na ujazo wa nusu kilo ambapo jeshi polisi linaendelea na uchunguzi ili kujua thamani halisi ya dawa hizo.