Alhamisi , 24th Mei , 2018

Mwakilishi wa Jimbo la Paje, Jaku Hashim Ayoub ameitaka serikali kuchukua hatua za kuwadhibiti waajiri wanaojihusisha na vitendo vya kuwaomba wanawake rushwa ya ngono kwenye ajira.

Mwakilishi huyo ameyasema hayo katika kikao cha Baraza la Wawakilishi wakati akiuliza swali lake la msingi kuhusu wanawake kudaiwa rushwa ya ngono na wanatakiwa wafanye nini wanapokutana na kadhia hiyo.

Akijibu swali la hilo, Naibu Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto, Shadia Mohammed amesema serikali haina takwimu za matukio hayo kwa kuwa wanawake wengi hawaelewi rushwa ya ngono ila viashira huwa vinaonekana na hushindwa kuripoti vitendo hivyo.

"Wanawake wanashindwa kuripoti matukio hayo kwa kuwa wanahofia kuachishwa kazi au kukosa kazi, kwa kawaida rushwa ya ngono hufanyika kwa siri sana tofauti na rushwa nyingine na hufanywa kwa lengo la kupandishwa cheo, mshahara au msaada wowote katika kazi", amesema Shadia.

Aidha, Shadia amesema serikali inaendelea kutoa elimu ya rushwa ili kujenga uelewa wa dhana na maana halisi ya rushwa na kuepukana na matendo hayo.

Kwa upande mwingine, Naibu Waziri huyo amewataka wanawake wanaokumbana na kadhia hiyo kuenda kuripoti Polisi pamoja na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa Zanzibar ili kudhibiti matukio hayo.