Jumatano , 19th Feb , 2025

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, ameonya vikali wanachama wanaotafuta uteuzi wa udiwani, uwakilishi na ubunge kwa njia zisizo halali, akisisitiza kuwa chama hakitasita kuwaengua wale watakaokiuka Katiba, Kanuni na maadili ya CCM kuelekea Uchaguzi

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi

Akizungumza jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa makatibu wa matawi na kata kutoka Wilaya ya Dodoma, Balozi Nchimbi alisema baadhi ya wanachama wameanza kampeni kabla ya muda rasmi kwa kutumia mbinu kama kuanzisha mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), kufadhili matukio ya kijamii kama kumbukumbu za misiba na sherehe za ndoa, pamoja na kushinikiza vikao vya chama kuwapitisha bila kupingwa.

"Tayari tumeshuhudia baadhi ya wabunge na madiwani wakitafuta mbinu za kuhakikisha wanapitishwa bila kupingwa. Wengine wanahamasisha matamko ya vikao, huku baadhi wakihudhuria matukio yenye lengo la kujitambulisha mapema kwa wapiga kura. Wapo wanaowapa posho wahudhuriaji wa mikutano wakiwa wamevaa sare za CCM ili kuonesha wanaungwa mkono. Tunawataka waache mara moja. CCM ina mfumo madhubuti wa kufuatilia mwenendo wa wanachama wake, na kumbukumbu hizi zote zinahifadhiwa. Wanaweza kushangaa majina yao yakiwekwa pembeni," alisema.

Balozi Nchimbi aliwataka madiwani na wabunge walioko madarakani kuacha kupuuza majukumu yao kwa kisingizio cha maandalizi ya uchaguzi, akisema chama kitafanya tathmini kwa kila mgombea kulingana na utendaji wake, si kwa uwezo wa kutoa fedha kwa wapiga kura.