
Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dkt. Leonard Maboko akizungumza na wadau mbalimbali walio katika Mapambano dhidi ya Ukimwi leo jijini Dar es salaam. Mkurugenzi huyo amekutana na wadau hao kwa mara ya kwanza kuzungumza nao kuhusu mikakati mbalimbali ya kudhibiti Ukimwi.
Akizungumza katika kikao chake cha kwanza na wadau mbalimbali walio katika mapambano dhidi ya Ukimwi leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dkt. Leonard Maboko amesema kuwa baadhi ya wadau, mashirika na taasisi zimekuwa zikifanya shughuli nje ya malengo ya awali ya kuanzishwa hali inayosababisha mgongano katika jamii.
"Zipo baadhi ya taasisi zinazofanya shughuli nje ya malengo, tunatambua Serikali haijakataa jitihada za makundi mbalimbali ya kupambana na UKIMWI, sisi kama TACAIDS tutaendelea kuungana na Serikali kuhakikisha kuwa zile taasisi zilizo kwenye mapambano zinasimamia malengo ya kuanzishwa kwake na si vinginevyo" Amesisitiza Dkt. Maboko.
Amewataka wadau na mashirika hayo kuendelea kujikita na kuongeza nguvu katika utoaji wa elimu ,uhamasishaji wa wananchi kupima kwa hiari VVU kwa lengo la kujua hali zao ili waweze kujikinga na maambukizi mapya ya ugonjwa huo.
Pia amewata wadau hao kuangalia namna bora ya kuwafikia, kuwaelimisha na kuwafuatilia wananchi walio katika makundi maalum kwenye mazingira hatarishi pia kuongeza shughuli za utafiti zitakazoisaidia nchi kufikia lengo la maabukizi sifuri.
Amesema hali ya uelewa wa wananchi juu ugonjwa wa Ukimwi imefikia asilimia 90 kwa kuwa watanzania sasa wanauelewa kuhusu ugonjwa huo na hali zao . Aidha, wengi wana uelewa iwapo wamepata maambukizi au la kutokana na kuongezeka kwa kampeni za uhamasishaji na elimu ya kujikinga na maambukizi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Chama cha Uzazi na Malezi Bora Tanzania (UMATI), Lulu Ng’wanakilala amesema Taasisi zinazosajiliwa kutoa huduma za kuzuia na kupunguza maambukizi dhidi ya Ukimwi kujiingiza kwenye shughuli za uanaharakati zinakwamisha na kupunguza juhudi za Serikali na wadau wengine walio kwenye mapambano dhidi ya Ukimwi.
‘Sisi kama wadau wa hizi taasisi tunaongea lugha moja, NGOs zinazosajiliwa kutoa huduma na kuanza kufanya uanaharakati kupitia masuala ya Ukimwi zinakwenda kinyume cha malengo, sisi tupo kwa lengo moja kuhakikisha maambukizi yanafikia sifuri kuhakikisha wote wanaotakiwa kupata huduma wanafikiwa na huduma zetu hasa makundi yanayochangia kwa kiasi kikubwa maambukizi ya Ukimwi’ Amesisitiza.