Jumatano , 9th Jun , 2021

Mkuu wa wilaya ya Bukoba mkoani Kagera Deodatus Kinawiro amepiga marufuku vitendo vya wananchi kuwatishia kwa mapanga mafundi wanaotandaza mabomba ya maji katika kijiji cha Rwagati kata ya Kemondo Bukoba Vijijini.

Mkuu wa wilaya ya Bukoba mkoani Kagera Deodatus Kinawiro

Ameongeza kuwa watakaorudia vitendo hivyo watachukuliwa hatua za kisheria maana kufanya hivyo ni kosa la jinai.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ikiwamo ya maji, mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa serikali imeweka gharama kubwa ya shilingi bilioni 14.8 kwa ajili ya kuhakikisha inaondoa kero ya maji kwa wananchi wa kata Kemondo na vijiji jirani, na kwamba ili mradi huo utekelezwe kwa ufanisi  wananchi wanapaswa kutoa maeneo yao kidogo kwa ajili ya kupitisha mabomba.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kijiji Rwagati ulikotokea mtafaruku huo Yahya Nuru amesema kuwa wananchi wake walilalamikia mafundi hao kukata migomba yao katika maeneo ambayo hawakukubaliana awali lakini akadai kwa sasa wamekwishakubali kutoa maeneo yao kuruhusu mabomba ya maji yapite, huku mmoja wa wananchi akidai hana mgogoro tena na mafundi hao.