Jumatatu , 11th Nov , 2024

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, ameeleza kwamba mpango mpya wa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu utaimarisha usalama wa fedha za serikali huku ukihakikisha marejesho yanafanyika kwa ufanisi. 

Mabelya ametoa kauli hiyo tarehe 11 Novemba 2024, katika Kongamano la Uelimishaji na Uhamasishaji Jamii Juu ya Uwepo wa Mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu Sambamba na Matumizi ya Nishati Safi linalofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo.

Katika hotuba yake, Mabelya ameeleza kwamba miaka ya nyuma utoaji wa mikopo kupitia halmashauri ulikumbwa na changamoto nyingi, hususan katika urejeshaji wa mikopo hiyo. Amesema kuwa wajasiriamali walikuwa wakijiunga kwenye vikundi lakini walishindwa kudumisha biashara zao, na hivyo kukumbwa na madeni makubwa ambayo yaliathiri sio tu maisha yao binafsi bali pia familia zao. 

"Mwisho wa siku, mkopo ni lazima urejeshwe, na changamoto hizo zimekuwa mzigo mkubwa kwa wananchi wetu," amesema Mabelya.

Kwa kutambua changamoto hizo, Mabelya amesema Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan aliona haja ya kuleta mabadiliko katika utaratibu wa utoaji wa mikopo hii. Mabelya amebainisha kuwa, sasa, mikopo hiyo itatolewa kupitia benki badala ya mfumo wa awali uliotumia halmashauri moja kwa moja. 

"Kwa halmashauri yetu ya Jiji la Dar es Salaam na Wilaya ya Ilala, tumeteuliwa kuwa miongoni mwa halmashauri 10 za mfano nchini, ambapo mikopo hii sasa itatolewa kwa njia ya kibenki. Hatua hii inalenga kulinda fedha za serikali na kuimarisha utaratibu wa marejesho," amesisitiza.

Mabelya ameongeza kuwa mfumo huu mpya pia unatoa uhakika kwamba mkopaji ni mshiriki halali wa vikundi vilivyoidhinishwa, huku utaratibu wa marejesho ukiwa wazi zaidi ili kuepusha madeni yasiyolipika. "Tangu mwezi Julai mwaka huu, dirisha la utoaji mikopo limefunguliwa rasmi. Tumefanya mafunzo kwa wataalamu wetu na kwa wananchi katika kata zote 36 za Wilaya ya Ilala," amesema.

Mabelya ameelezea zaidi kwamba mafunzo hayo yamekuwa yakifanyika katika ngazi ya kata ili kuhakikisha wananchi wanapata uelewa mzuri kuhusu matumizi ya mikopo hiyo. Amemshukuru Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, kwa kujitokeza kuwa mgeni rasmi katika kuzindua kongamano hili la siku mbili. 

"Tumesema hatuwezi kuanza kutoa mikopo bila ya wananchi hawa kufahamu utaratibu mpya. Tumefanya kazi kubwa ya uelimishaji, na tunaamini sasa wananchi wako tayari kukopa, kuanzisha biashara, na kuhakikisha marejesho yanafanyika ipasavyo ili fedha hizo ziwanufaishe wengine," amesema Mabelya.

Katika hotuba yake, Mabelya amempongeza Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuinua uchumi wa wananchi kupitia mikopo hii.

 "Hii ni hatua muhimu sana kwa Jiji la Dar es Salaam kwani itasaidia kuunda msingi imara kwa wajasiriamali ambao wataendelea kukua na kuwa wafanyabiashara wa kati na hatimaye kuwa wafanyabiashara wakubwa kama wale tunaowashuhudia sasa," amesema.

Kongamano hilo linalenga kutoa dira na mwongozo kwa wananchi kuhusu fursa za mikopo na jinsi ya kuitumia kwa faida ya kuimarisha maisha yao. Siku ya kwanza ya kongamano hilo imeshuhudia ari kubwa kutoka kwa wananchi ambao wamejifunza na kuahidi kushiriki kikamilifu katika mpango huo mpya wa mikopo kwa ajili ya kujikomboa kiuchumi.