Ijumaa , 11th Sep , 2015

Serikali inatarajia kuwagawia wananchi ekari 7000 za ardhi, zilizonyanganywa kwa muwekezaji toka nje wa mashamba ya Tanzania Plantation Limited, ili kuweza kutatua mgogoro wa ardhi mkoani Arusha.

Taarifa hiyo imetolewa na waziri wa Ardhi, Nyumba na makazi William Lukuvi alipokuwa akiongea na waandishi wa habari mkoani Arusha, akitoa taarifa ya usuluhishi wa mgogoro wa ardhi katika miko ya Arusha na Manyara,

Waziri Lukuvi amesema kwamba mashamba hayo yamekuwa na mgogoro kwa muda mrefu kati ya mwekezaji na wananchi, hivyo kutokana na uhitaji mkubwa wa ardhi kwa wananchi, wameamua kuyabatilisha mashamba hayo na kukusudia kuyagawa kwa wananchi.

'Nimekuja Arusha na timu yangu ambayo itafanya uhakiki wa watu 2000 wenye uhitaji na baada ya kujiridhisha watafanya zoezi la ugawaji, na pia watu watapewa hati ya kumiliki ardhi zao, safari hii hatutagawa ardhi kienyeji", alisema Waziri Lukuvi.

Waziri Lukuvi aliendelea kwa kusema kwamba baada ya ubatilishwaji huo Arusha imepata ekari 6,176.5, na Halmashauri ya Meru imepata hekari 925, hivyo kufanya kufikia hekari 7,101, ambazo ndizo zitagawanywa kwa wananchi.

Mbali na mashamba hayo Waziri Lukuvi amesema pia wamepata ekari 100 toka kwa shamba la Imani Estate na shamba la Noors lenye ekari 2296, lililokuwa na mgogoro kwati ya mwekezaji na wananchi wa kijiji cha Laroi na Kisima cha Mungu, litagaiwa kwa wananchi baada ya mazungumzo kati ya mwekezaji kukubali kuachia shamba hilo.

Jumla ya migogoro 80 ya ardhi iliyowasilishwa kwa waziri Lukuvi kutoka katika Halmashauri ya jiji la Arusha, Halmashauri ya wilaya ya Arusha na Halmashauri ya Wilaya ya Meru, imepatiwa ufumbuzi hivyo kupunguza migogoro ya ardhi iliyokuwa ikilisakama jiji hilo.