
Wapiganaji saba wa kundi la wanamgambo la Al Shabab waliotekeleza shambulio jipya la kigaidi jana Jumamosi, Oktoba 4 huko Mogadishu, nchini Somalia baada ya kuvamia jengo kuu la magereza wameuawa kufuatia mapigano ya saa moja, serikali ya Somalia imesema.
Kundi la al-Shabab lilifanya shambulizi katika gereza la chini ya ardhi linalojulikana kama Godka Jilow lenye ulinzi mkali, katikati mwa mji mkuu, Mogadishu wakati gari lililokuwa na vilipuzi na kupambwa kwa rangi za idara za usalama za nchi hiyo likiendeshwa kwa kasi kabla ya kulipuka.
Serikali ilisema shambulio hilo lilianza kwa mlipuko wa bomu lililokuwa kwenye gari hilo, na kufuatiwa na kurushiana risasi na milipuko ambayo ilitanda katika jiji lote, huku askari watatu wa vikosi vya usalama wakiuawa pia wakati wa juhudi za kuzima shambulio hilo.
Katika taarifa, al-Shabab, tawi la al-Qaeda, lilisema lilianzisha shambulio hilo ili kuwakomboa baadhi ya wanachama wake kutoka katika gereza hilo . Afisa mmoja wa usalama wa Somalia katika gereza hilo aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba walisikia mlipuko mkubwa kwenye lango la seli na punde milio ya risasi ikaanza.
Shambulio hilo lilitokea saa chache baada ya serikali kufungua tena makumi ya barabara katika mji mkuu kwa mara ya kwanza katika kipindi cha muongo mmoja, huku Waziri Mkuu Hamza Barre akitaja "mabadiliko yanayoonekana na maboresho" katika hali ya usalama.
Somalia, nchi maskini na isiyo na utulivu katika Pembe ya Afrika, imekumbwa na mashambulizi mapya ya Al Shabab, kundi ambalo wanamgambo wake wana mafungamano na Al-Qaeda. Waasi hao wamechukua udhibiti wa makumi ya miji na vijiji tangu kuanza mashambulizi yao mapema mwaka huu, na kufuta karibu mafanikio yote yaliyopatikana kwa serikali ya Somalia wakati wa operesheni yake ya kijeshi ya mwaka 2022 na 2023.
Nchi hiyo imekuwa ikipigana na Al Shabab tangu katikati ya miaka ya 2000. Lakini hali ya usalama imezorota sana mwaka huu ambapo mapema mwaka huu waasi hao walidai kuhusika na mlipuko wa bomu ambao uliukosa msafara wa rais mnamo Machi 18 na kurusha makombora kadhaa karibu na uwanja wa ndege wa Mogadishu mapema mwezi Aprili.