Jumanne , 28th Jun , 2016

Wanakijiji wa kijiji cha Lukonde kata ya Mkuyuni, mkoani Morogoro wanamuomba Waziri wa Ardhi, Nyumba na maendeleo ya makazi William Lukuvi
aingilie kati mgogoro wa ardhi unaoendelea kijijini hapo kati ya wanakijiji na muwekezaji.

Akiongea na waandishi wa habari kwa niaba ya wananchi wenzie 824 leo jijini Dar es Salaam, Bi. Mary Sanga amesema kuwa hapo awali waziri alishindwa kuingilia kati suala hilo kutokana na kesi kuwa mahakamani lakini hivi sasa kesi imemalizwa bila ya wao kuelewa imemalizwaje kwani hawajakabidhiwa hukumu ya kesi.

Bi Mary amesema kuwa walipewa maelekezo na mhudumu wa mahakama kuu kuwa wao wameshindwa kesi hiyo waliokuwa wanadai umiliki wa eneo lao lenye ukubwa wa hekari 2,700 bila ya kuelewa imemalizwaje ndipo wameamua kujitokeza mbele ya vyombo vya habari kumuomba waziri Lukuvi awasaidie.

Aidha, amebainisha kuwa serikali iangalie upya suala la hati miliki kutumika kama kigezo cha kupata haki kwani ndio kigezo kinachotumika na watu wachache kuwanyang`anya haki wazaliwa wa sehemu husika.