Jumapili , 15th Oct , 2023

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene amesema mtu aliyemaliza kidato cha nne ana uwezo mkubwa wa kuchambua mambo kisayansi ukilinganisha na yule wa darasa la saba ambapo amewasihi wanafunzi kusoma kwa bidii

Simbachawene ametoa nasaha hizo wakati wa mahafali ya 19 kwa wanafunzi wa  kidato cha nne  katika shule ya Sekondari ya Rudi iliyopo katika Kata ya Rudi, Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma.

Ameongeza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt. Samia Suluhu Hassan amelenga kuboresha elimu na kuifanya elimu ya kidato cha nne  kuwa ya lazima na sio hiyari na hivyo, wananchi wa jimbo la Kibakwe wananufaika pia na maono hayo.

“Ninawaomba wananchi wote wa Jimbo la Kibakwe kupitia kwenu ninyi wazazi wa watoto hawa wanaofanya mahafali yao leo, kutambua kuwa mtu aliyemaliza kidato cha nne ana uwezo mkubwa wa kuchambua mambo kisayansi ukilinganisha na yule wa darasa la saba. Hivyo elimu ni muhimu kwa kuwa inaongeza uwezo wa kufikiri na kupanua uelewa wa namna bora ya kupambana na changamoto” alisisitiza.

Aidha, amewataka wazazi kushirikiana na walimu katika kulea vijana hao wakati wote wanapokuwa shuleni kwa kuwa takwimu zinaonesha ni wanafunzi 64 tu kati ya wanafunzi 174 walioanza kidato cha nne mwaka 2020  ndio wamefanikiwa kumaliza kidato cha nne.

Kufuatia hatua hiyo Mhe.Simbachawene amewataka wazazi kuwahimiza watoto wao kutambua umuhimu wa elimu ili kuwa na jamii yenye uelewa kwa faida ya wananchi wa Kata  ya Rudi na Taifa kwa jumla.

Awali, Mkuu wa shule hiyo ya Rudi, Happy Mulio amesema licha ya shule hiyo kufanya vizuri lakini imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutokuwa na maji ya uhakika pamoja na hosteli kwa wanafunzi wa kike hali inayowapelekea wanafunzi hao kukaa mtaani ambapo wamekuwa wakikumbana na changamoto ikiwemo kupata ujauzito.