Ofisa elimu Mkoa wa Dodoma, Juma Kaponda.
Hayo yamebainika jana katika ziara ya kushtukiza ya Ofisa elimu Mkoa wa Dodoma, Juma Kaponda aliyoifanya katika wilaya hiyo na kujionea hali halisi ya ukosefu wa wanafunzi katika shule za sekondari za kata za Ving’awe, Lupeta na Kimagai zilizopo wilayani humo.
Hali ya utata ilianzia katika shule ya Sekondari ya Ving’awe ambapo jumla ya wanafunzi waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza mwaka huu ni 80 lakini waliokuwemo darasani ni wanafunzi watano tu.
Ambapo katika shule ya Sekondari Lupeta wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza ni 88 lakini waliokuwemo darasani ni saba tu na katika shule ya sekondari ya Kimagai jumla ya wanafunzi 106 walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza lakini walikuwemo darasani ni wanafunzi sita tu.
Kwa hiyo kufanya jumla ya wanafunzi 18 tu waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu katika sekondari hizo tatu kuwasili shuleni huku wengine 256 wakibaki nyumbani kwa sababu mbalimbali.
Kutokana na hali ya mahudhurio ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika kata hizo kutoridhisha, Afisa elimu huyo aliamua kukutana na viongozi wa vijiji, watendaji, waalimu pamoja na kamati za shule kwa vikao vya dharura ili kujua tatizo liko wapi.
Akikataa jina lake kutajwa gazetini mmoja wa waalimu anayefundisha katika shule hizo amesema kuwa sababu kubwa ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kutofika shuleni ni pamoja na baadhi ya wazazi wao kutokuwa na uwezo wa kuwahudumia watoto wao kwa kuwapatia mahitaji yao muhimu kwa ajili ya kuendelea na masomo.
“Tatizo kubwa hapa mimi ninaloliona ni uwezo mdogo wa wazazi kushindwa kuwahudumia watoto wao kwa kuwalipia ada, sare za shule pamoja na michango mingine inayohitajika kwa mwanafunzi kujiunga na kidato cha kwanza.” Alisema mwalimu huyo.
Hata hivyo Kaponda amewaagiza watendaji wa kata na vijiji kwa kushirikiana na kamati za shule kufanya msako mkali wa kuwasaka wazazi wa wanafunzi hao na kuhakikisha kuwa watoto hao wanarejea shuleni mara moja ili kuendelea na masomo yao.
Kaponda ametoa siku saba za wanafunzi hao kurejea shuleni pasipo a visingizio vyovyote kutoka kwa watoto, walezi pamoja na wazazi.
Aidha ameiagiza kamati ya ulinzi na usalama ya kata na kijiji kuhakikisha kuwa watoto wote wanaotakiwa kuwepo shuleni wanakwenda shuleni bila kukosa.
Mbali na hilo amewaagiza wakuu wa shule kuwaacha watoto ambao hawajalipa ada kutokana na wazazi wao kukabiliwa na msimu wa kilimo kuwaacha watoto hao waendelee na masomo bila kufukuzwa shule kwani jukumu la kulipa ada ni la mzazi na si la mwanafunzi.