Jumatatu , 16th Mei , 2022

Wanafunzi 76 katika shule ya sekondari ya wasichana Mkuza iliyopo Kibaha mkoani Pwani, inayomilikiwa na kanisa la KKKT wamenusurika kupoteza maisha baada ya moja ya bweni la shuleni hapo kuteketea kwa moto uliozuka usiku wa kuamkia leo Mei 16, 2022, wakati wanafunzi hao wakiwa katika ibada

Bweni la shule ya sekondari ya wasichana Mkuza lililoungua

Akielezea mazingira ya ajali hiyo mara baada ya kufika katika eneo la tukio hilo, Mkuu wa mkoa wa Pwani Alhaj Aboubakar Kunenge, amesema wakati ajali hyo inatokea kulikuwa na mwanafunzi mmoja ndani ya bweni ambaye hakuungana na wenzake kwenda kwenye ibada kutokana na kukabiliwa na maradhi lakini aliokolewa na hakuna mwanafunzi aliyejeruhiwa.

Nao uongozi wa shule hiyo ukiongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la KKKT Dkt. Alex Malasusa, ameishukuru serikali, Jeshi la Zimamoto pamoja na wananchi kwa ushirikiano walioutoa na kufanikisha wanazima moto huo ili kuondoa madhara makubwa ambayo yangeweza kujitokeza.