Alhamisi , 10th Nov , 2016

Takribani wanafunzi 30,000 nchini Tanzania wameepuka adha ya kukaa chini baada ya taasisi ya Hassan Maajar kugawa madawati elfu tisa kwa shule za msingi na sekondari katika mikoa 13 nchini kupitia programu yake ya kuboresha mazingira ya elimu nchini.

Bw. Daniel Mwasandube (kulia), Mwenyekiti wa Kamati ya Uchangishaji Fedha

 

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchangishaji Fedha wa taasisi hiyo Bw. Daniel Mwasandube, amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia hafla nyingine ya uchangishaji fedha kwa ajili ya elimu, hafla itakayofanyika jijini Dar es Salaam Novemba 23 mwaka huu.

Kwa mujibu wa Bw. Mwasandube, sehemu kubwa ya madawati hayo wamefanikiwa kupitia ufadhili wa Benki M ya jijini Dar es Salaam ambao katika kipindi cha takribani miaka mitano wamekuwa wakifadhili mradi huo wa uboreshaji wa mazingira ya elimu.

"Juhudi setu zimefanikiwa kuhamasisha umma nchini na kwingineko kutambua umuhimu wa kusaidia sekta ya elimu chini ya kauli mbiu ya 'Dawati Kwa Kila Mtoto' ," amesema Bw. Mwasandube.

Ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitano ya mradi huo, jumla ya shilingi bilioni 1.7 zimekusanywa na kuelekezwa moja kwa moja katika miradi husika na wanajisikia fahari kuona idadi kubwa ya wanafunzi hivi sasa wanaketi kwenye madawati kupitia programu yao hiyo.