Jumanne , 6th Dec , 2016

Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemuagiza Waziri na Katibu Mkuu katika Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kusitisha mara moja utekelezaji wa zoezi la kuwaondoa wafanyabiashara wadogo (Machinga) katika jiji la Mwanza.

Rais John Magufuli

Rais Magufuli amesitisha zoezi hilo kwa muda mpaka hapo mamlaka husika itakapokamilisha maandalizi ya maeneo watakapohamishiwa na kwa kuwashirikisha wamachinga wenyewe.

Rais Magufuli akiwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa agizo hilo leo Ikulu Jijini Dar es Salaam huku akionya kuwa kiongozi yeyote ambaye hayupo tayari kutekeleza agizo hilo aachie ngazi.

"Kumeibuka tabia ya Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kuwafukuza Wamachinga bila utaratibu wowote wa wapi wanawapeleka na wakati mwingine wanapelekwa maeneo ya mbali ambayo hayafai hata kwa kufanyabiashara, hili jambo siyo sawa hata kidogo".

Vurugu za Machinga Jijini Mwanza

"Sipendi Wamachinga wafanye biashara kwenye hifadhi ya barabara lakini hakuna sheria katika nchi hii inayosema mtu wa biashara ndogondogo au Mmachinga hatakiwi kukaa katikati ya mji, tukianza kwenda kwenye utaratibu wa namna hiyo maana yake tunaanza kutengeneza  madaraja ya Watanzania, kwamba kuna Watanzania fulani wa daraja fulani wanapaswa kukaa katikati ya mji na Watanzania wa daraja fulani hawatakiwi kukaa katikati ya mji, huo sio mwelekeo wetu na wala Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ambayo mimi na wewe (Makamu wa Rais) tulipita kuinadi, haisemi tutengeneze madaraja ya watu wanaostahili kukaa mjini na wengine hawastahili kukaa mjini, sasa nimeona hili nilizungumze na nataka kulirudia kwa mara ya mwisho" amesema Rais Magufuli.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana - Mary Tesha

Dkt. Magufuli ameelekeza kuwa Wamachinga walioondolewa katika maeneo yao Jijini Mwanza waachwe waendelee na shughuli zao mpaka hapo Halmashauri ya Jiji la Mwanza itakapokamilisha maandalizi ya mahali watakapohamishiwa na kwa kuwashirikisha Wamachinga wenyewe.

"Narudia na hii ni mara ya mwisho, kawaambieni hata Wamachinga wa Mwanza warudi kwenye maeneo yao mpaka watakapowatengenezea utaratibu mzuri, Kigamboni hapa palikuwa na wamachinga eneo fulani wamehama vizuri kweli, wakatengenezewa miundo mbinu yao katika soko lao na sasa hivi wanafanya kazi vizuri, na waliwashirikisha viongozi wa Wamachinga, lakini Mwanza imekuwa ni amri tu na wengine wanatumia hata msemo wa Hapa Kazi Tu, mimi sikusema msemo wa Hapa Kazi Tu wa namna hiyo, nadhani mmenielewa" amesisitiza Rais Magufuli alipokuwa akiwaekeleza Naibu Waziri wa TAMISEMI Mhe. Suleiman Jafo na Katibu Mkuu TAMISEMI Mhandisi Mussa Iyombe.

Vurugu za Machinga walioondolewa katikati ya Jiji la Mwanza