Alhamisi , 12th Jun , 2014

Washtakiwa watatu waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka mawili ya kula njama na kumfanyia vitendo vya ukatili mtoto Nasra Rashid Mvungi, wamefunguliwa mashtaka ya mauaji.

Watuhumiwa wakiwa mahakamani

Washtakiwa watatu waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka mawili ya kula njama na kumfanyia vitendo vya ukatili mtoto Nasra Rashid mvundi, wamefutiwa mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili na mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa morogoro na badala yake kupandishwa upya kizimbani wakikabiliwa na mashtaka ya mauaji.

Waendesha mashtaka wamedai kuwa mashtaka hayo ya awali yamefutwa na mahakama baada ya aliyefanyiwa matendo hayo kufariki dunia, badala yake washtakiwa hao sasa wanakabiliwa na shtaka la mauaji.

Hakimu Mary Moyo amesema washtakiwa hao hawatakiwi kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kukosa mamlaka ya kisheria kusikiliza kesi za mauaji na kutokana na shtaka hilo kutokuwa na dhamana wote walipelekwa rumande hadi Juni 26 kesi hiyo itakapofikishwa mahakamani hapo kwaajili ya kutajwa.

Washtakiwa hao Mariam Said, ambaye ni mama mkubwa wa marehemu, Mtonga Omary baba mkubwa na Rashid Mvungi ambaye ni baba mzazi wa Nasra.