Alhamisi , 29th Jul , 2021

Zaidi ya wanafunzi 130 wa kidato cha kwanza hadi cha nne katika shule ya sekondari Tabasamu, iliyopo Nyasaka, Ilemela mkoani Mwanza, wamekosa masomo kwa kipindi cha miezi sita baada ya walimu kugoma kuingia darasani kufundisha wakishinikiza uongozi wa shule hiyo kuwalipa stahiki zao.

Kushoto ni Mwalimu George Giseli na kulia ni Velina Mashaka, baadhi ya walimu walioeleza changamoto yao.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wa shule hiyo ambao wanadaiwa kukosa masomo kwa kipindi cha miezi sita Mwanafunzi Sarafina Lucas, amesema wamekosa masomo kwa muda mrefu hivyo akaiomba serikali kupitia Wizara ya Elimu kuingilia kati suala hilo ili waweze kuendelea na masomo.

Kwa upande wake Mkuu wa shule hiyo Marwa Chacha, amesema kuwa ni kweli shule hiyo inakabiliwa na changamoto ya walimu kutolipwa mishahara yao lakini jambo hilo linashughulikiwa.

Jitihada za kumtafuta Mkurugenzi wa shule hiyo Patrick Masai, ili aweze kutoa majibu yanayohusiana na shule hiyo hazikuzaa matunda, baada ya kupatikana na kudai kuwa yuko safarini.