Jumatano , 25th Jan , 2023

Wakuu wote wa wilaya tano za mkoa wa Dar es Salaam, wamehamishwa na kupelekwa kwenye wilaya za mikoa mingine nchini Tanzania.

Waliokuwa wakuu wa wilaya ndani ya jiji la Dar es Salaam

Taarifa ya wakuu hao wa wilaya kuhamishwa imetolewa hii leo Januari 25, 2023, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan, amemhamisha aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo kwenda kuwa Mkuu wa wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.

Aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Kinondoni Godwin Gondwe, amehamishwa na kupelekwa mkoani Dodoma kwenda kuwa Mkuu wa wilaya ya Bahi.

Fatma Nyangasa aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Kigamboni amepelekwa mkoani Pwani kwenda kuwa Mkuu wa wilaya ya Kisarawe.

Aidha aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Ilala Ng'wilabuzu Ludigija, amehamishiwa mkoani Mwanza kwenda kuwa Mkuu wa wilaya ya Kwimba.

Na mwisho aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Ubungo Kheri James, amehamishwa na kupelekwa mkoani Manyara kwenda kuwa Mkuu wa wilaya ya Mbulu.

Kwa ujumla wake Rais Samia Suluhu Hassan, ameteua wakuu wa wilaya wapya 37 huku 55 wakibaki kwenye wilaya zao na wengine 48 wamehamishwa wilaya. Idadi hiyo inafanya kuwa jumla yao kuwa wakuu wa wilaya 140 ambapo kati yao wanaume ni 100 na wanawake ni 40.