Leo Septemba 23, Mahakama hiyo imewaachia huru washtakiwa watano waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwa makosa ya kujiunganishia bomba la mafuta ambalo ni mali ya Mamlaka ya Bandari nchini (TPA) kinyume cha taratibu.
Uamuzi huo umefikiwa mara baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) kuieleza Mahakama kuwa hana nia ya kuendelea na kesi hizo.
Walioachiwa huru na mahakama hiyo ni Audai Ismail (43) mkazi wa Kibaha, Chibony Emmanuel, Roman Abdon, Amina Shaban na Zubery Ally.
Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama hiyo Januari 16, 2019, kujibu mashtaka matatu likiweno la kujiunganishia isivyo halali bomba la mafuta mali ya TPA, ambapo kwa pamoja wanadaiwa kati ya mwaka 2015 hadi Januari 2018 katika eneo la Tungi Muungano Wilayani Kigamboni, wanadaiwa kujiunganishia bomba la mafuta ya Dizeli
lenye upana wa inchi moja kutoka katika bomba lenye upana wa inchi 24 bila kibali.
Shtaka la pili lilikuwa ni la kuharibu miundombinu kwa madai ya kuwa walitoboa bomba hilo ambalo lilikuwa likitumika kusafirisha mafuta, pamoja na kudaiwa kuharibu bomba la mafuta mazito lenye upana wa inchi 28 la kusafirishia mafuta ghafi.