Watanzania leo wameadhimisha miaka 53 ya uhuru wa Tanganyika ambayo mwaka 1964 iliungana na Zanzibar na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Maadhimisho hayo yamefanyika kitaifa jijini Dar es salaam katika uwanja wa Taifa ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu Mheshimiwa Jakaya Kikwete.
Sherehe za maadhimisho hayo zimepambwa na gwaride lililoandaliwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ambalo pia lilivishikisha vikosi vya Jeshi la Kujenga Taifa-JKT, Polisi na Magereza.
Wakati huo huo Rais Jakaya Kikwete ametoa msamaha kwa wafungwa 4969, wakiwemo 4082 ambao wamepunguziwa adhabu zao na 887 ambao wataachiwa huru.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema wafungwa watakaonufaika na msamaha huo kuwa ni wenye magonjwa kama UKIMWI, Kifua Kikuu, Saratani walio katika hali mbaya, wazee wenye umri wa 70 au zaidi, umri ambao utapaswa kuthibitishwa na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa mganga mkuu wa mkoa au wilaya.
Wengine ni wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani pamoja na wale walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya, wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili ambao utathibishwa na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa mhanga mkuu wa Mkoa au wilaya.
Wafungwa ambao hawatanufaika na msamaha huo ni pamoja na wale waliohukumiwa kunyongwa, waliohukumiwa kwa makosa ya kuomba na kupokea au kutoa rushwa na wale wanaotumikia kifungo kwa makosa ya unyang'anyi wa kutumia silaha.